Nenda kwa yaliyomo

Aral (ziwa)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ziwa Aral)
Meli ya ziwani inayokaa jangwani mahali pa bandari ya zamani.

Ziwa Aral (kwa Kikazakhi: Арал теңізі Aral tengizi, kwa Kiuzbeki: Orol dengizi, kwa Kirusi: Аральскοе мοре Aralskoye more) ni ziwa la Asia ya Kati, mpakani mwa Kazakhstan na Uzbekistan.

Hadi mwaka 1960 lilikuwa na eneo la maji la km² 68,000, lakini limepungua hadi kubaki na km² 17,160 pekee mwaka 2004. Tangu 1987 kupungua kwa maji kulisababisha ugawaji wa ziwa katika sehemu mbili upande wa kaskazini na upande wa kusini ambazo haziunganiki tena.

Mito mikubwa inayoingia na kubeba maji yake ni Amu Darya na Syr Darya na mito hii ilitumiwa katika mipango ya Umoja wa Kisovyeti kwa umwagiliaji wa mashamba makubwa ya pamba na mazao mengine. Miradi hiyo iliyoanzishwa katika mazingira yabisi iliendelea kwa miaka 30 hivi hadi kushindikana; maji yamepotea kwa wingi mashambani na katika mifereji kutokana na usimbishaji na kusababisha kupungua kwa mazao. Kiasi cha chumvi ardhini kiliongezeka sana jinsi ilivyo mara nyingi katika miradi ya umwagiliaji ya nchi za joto na kumaliza rutuba ya udongo.

Ziwa halikupokea tena kiasi chake cha maji, hivyo likapungua. Sehemu kubwa za eneo la ziwa la awali zimekuwa jangwa. Maji yaliyobaki yameharibika kutokana na majitaka ya viwanda na mbolea nyingi iliyosukumwa kutoka mashamba mitoni halafu ziwani.

Kuna mradi wa kuokoa angalau sehemu ndogo ya kaskazini. Ukuta ulijengwa kwa shabaha ya kuzuia upotevu wa maji katika jangwa la msingi wa ziwa la kale. Uwiano wa maji yamepanda tena katika sehemu hii ndogo.

Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Aral (ziwa) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.