Nenda kwa yaliyomo

Yohane wa Dameski

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Yohane wa Damasko.
Mt. Yohane wa Damasko

Yohane wa Dameski (kwa Kiarabu يوحنا ابن ﺳﺮﺟﻮﻥ Yuḥannā ibn Sarjūn) alikuwa mmonaki, padri na mwanateolojia kutoka Dameski, mji mkuu wa Siria (Damasko, 676? - Palestina, 749?).

Aling'aa kwa utakatifu na ubora wa mafundisho, akapambana kwa nguvu zote na kaisari Leo III, kwa maneno na kwa maandishi, ili kutetea uhalali wa heshima kwa picha takatifu. Kisha kujiunga na monasteri ya Mar Saba karibu na Yerusalemu, alijitosa kutunga tenzi takatifu hadi kifo chake [1].

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1883 Papa Leo XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Ni msimamizi wa wachoraji.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Desemba[2].

Ioannis Damasceni Opera, 1603

Alizaliwa Dameski mwaka 676 hivi, labda katika familia ya Kiarabu ya Kikristo. Baba yake alikuwa Sarjūn ibn Manṣūr. Babu yake, Manṣūr, alikuwa wa kwanza katika familia kupewa vyeo vikubwa chini ya utawala wa halifa Mu'awiya bin Abi Sufyan na wa waandamizi wake.

Baba yake pia alikuwa mwanasheria, akafuatwa na Yohane ambaye bado kijana alipata kuwa mshauri wa halifa wa Damasko na msimamizi wa mali yake.

Lakini baadaye kidogo huenda akahukumiwa na kukatwa mkono wa kushoto. Hapo (mwaka 700 hivi) alihama mji huo na kujiunga moja kwa moja na monasteri ya Mt. Saba, kati ya Bethlehemu na Yerusalemu, ambapo alipewa upadrisho.

Alihubiri na kuandika sana hadi kifo kilipompata huko Palestina akiwa na umri wa miaka 73 (mwaka 749 hivi).

Katika maandishi yake alikusanya mafundisho ya mababu waliomtangulia, yeye akiwa wa mwisho kati yao.

Kitabu chake maarufu zaidi kinaitwa Kuhusu Imani Sahihi. Pia ametuachia tenzi bora kwa ajili ya liturujia.

Alitumia nguvu zake zote hasa kutetea matumizi ya picha na sanamu takatifu katika Ukristo dhidi ya waliotaka kuziteketezakwa kushikilia makatazo ya Agano la Kale, lakini pia kwa kujilinganisha na Uislamu kwa malengo ya kisiasa.

Hoja zake zilitegemea hasa umwilisho wa Mwana wa Mungu tumboni mwa Bikira Maria. “Zamani Mungu, akiwa hana mwili wala sura, hakuchorwa kwa picha. Lakini, kwa kuwa sasa ameonekana katika mwili na kuishi kati ya watu, mimi nachora upande ule wa Mungu ulioonekana. Siabudu maada, bali Muumba wa maada ambaye alipata kuwa maada kwa ajili yangu, akakubali kuishi katika maada na kuniokoa kwa njia ya maada. Kwa hiyo sitaacha kuheshimu maada ile ambayo wokovu wangu umepatikana kwa njia yake. Ila siiheshimu kikamilifu kama Mungu! Ingewezaje kuwa Mungu kile kilichopewa kuwepo kutoka utovu wa vyote?.… Hata hivyo mimi naheshimu na kustahi pia maada nyingine yote iliyoniletea wokovu, kwa kuwa imejaa nguvu na neema takatifu. Je, mbao za msalaba uliobarikiwa mara tatu si maada?… Na je, wino, na kitabu kitakatifu sana cha Injili, si maada? Je, altare ya ukombozi inayotupatia Mkate wa uzima si maada?… Na, muhimu kuliko yote, je, mwili na damu ya Bwana wetu si maada? Basi, ama tunatakiwa kufuta umbile takatifu la vitu hivyo vyote, ama tunatakiwa kulikubalia mapokeo ya Kanisa heshima ya picha za Mungu na za marafiki wake ambao wametakaswa na jina walilopewa, na kwa sababu hiyo wanatawaliwa na neema ya Roho Mtakatifu. Basi, usiikosee maada: haitakiwi kudharauliwa, kwa sababu hakuna kilichofanywa na Mungu ambacho ni cha kudharauliwa”.

Hivyo Yohane alikuwa kati ya wale wa kwanza waliotofautisha ibada inayotupasa kwa Mungu tu na heshima inayoweza kutolewa kwa malaika na watakatifu wake na hata kwa picha zinazowachora, ambayo imestawi hasa katika Makanisa ya Mashariki hadi leo. Kwa jumla ni mtazamo mpya, chanya, juu ya ulimwengu: maada yenyewe inaweza kufanywa chombo cha neema kwa kuitiwa Roho Mtakatifu.

Alipewa ushindi na Mtaguso wa pili wa Nisea (787) baada ya kifo chake.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Wewe, Bwana, ulinitoa katika viuno vya baba yangu; wewe uliniunda tumboni mwa mama yangu; wewe ulinitoa mwangani, mtoto uchi, kwa kuwa sheria za umbile letu zinafuata daima amri zako.

Wewe uliandaa kwa baraka ya Roho Mtakatifu uumbaji wangu na maisha yangu, si kadiri ya matakwa ya mtu wala ya tamaa ya mwili, bali kadiri ya neema yako isiyosemeka.

Uliandaa uzazi wangu kwa matayarisho yanayopita sheria za umbile letu, ulinitoa mwangani kwa kunifanya mwanao, uliniandika kati ya wafuasi wa Kanisa lako takatifu lisilo na doa.

Umenilisha maziwa ya Kiroho, maziwa ya maneno yako ya Kimungu.

Umenitegemeza kwa chakula kizito cha Mwili wa Yesu Kristo, Mungu wetu, Mwanao pekee mtakatifu sana, umenilevya kwa kikombe cha Kimungu cha Damu yake itiayo uzima, aliyoimwaga kwa wokovu wa ulimwengu wote…

Sasa, Bwana, kwa njia ya kuhani wako umeniita nitumikie wanafunzi wako.

Sijui kwa mpango gani umefanya hivi; wewe tu unajua…

Unichunge, Bwana, na uchunge mwenyewe pamoja nami watu wengine, ili moyo wangu usiniinamishe kulia wala kushoto, bali Roho wako mwema unielekeze njia nyofu ili matendo yangu yafuate matakwa yako, na yayafuate kweli mpaka mwisho.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  • Brown, Peter Robert Lamont (2003). The rise of Western Christendom: triumph and diversity, A.D. 200-1000 (tol. la 2nd, illustrated). Wiley-Blackwell. ISBN 0631221387, 9780631221388. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • Butler, Alban; Jones, Kathleen; Burns, Paul (2000). Butler's lives of the saints: Volume 12 of Butler's Lives of the Saints Series (tol. la Revised). Continuum International Publishing Group. ISBN 0860122611, 9780860122616. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • Jameson (2008). Legends of the Madonna. BiblioBazaar, LLC. ISBN 0554334135, 9780554334134. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • Louth, Andrew (2002). St. John Damascene: tradition and originality in Byzantine theology (tol. la Illustrated). Oxford University Press. ISBN 0199252386, 9780199252381. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • McEnhill, Peter; Newlands, G. M. (2004). Fifty key Christian thinkers. Routledge. ISBN 0415170494, 9780415170499. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • Sahas, Daniel J. (1972). John of Damascus on Islam. BRILL. ISBN 9004034951, 9789004034952. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • Vila, David (2000). Richard Valantasis (mhr.). Religions of late antiquity in practice (tol. la Illustrated). Princeton University Press. ISBN 0691057516, 9780691057514. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help)
  • The Works of St. John Damascene. Martis Publishing House, Moscow. 1997. {{cite book}}: Cite has empty unknown parameter: |1= (help)

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]