Nenda kwa yaliyomo

Viungo vinavyosafisha mwili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Viungo Vinavyosafisha Mwili (kwa Kiingereza Excretory Organs) ni viungo katika mwili wa binadamu na wanyama ambavyo vinahusika katika utoaji wa taka mwilini.

Binadamu kama viumbe hai wengine wanahitaji kutoa uchafu. Hakuna mfumo maalumu katika mwili wa binadamu ambao unahusika moja kwa moja katika utoaji wa uchafu kama vile kwa mfano mfumo wa upumuaji ambao unahusika moja kwa moja na upumuaji.

Viungo mbalimbali kutoka katika mifumo mingine kwa pamoja huweza kufanikisha suala la kusafisha mwili. Mfano viungo kama mapafu, mafigo na ngozi ambavyo vipo katika mifumo mingine hutumika katika mpangilio uliotajwa kutoa hewa chafu, mikojo na jasho.

Viungo hivyo hufanya kazi nyingine pia, zaidi ya utoaji taka, kwa mfano ngozi huhusika pia na kutunza joto la mwili na kadhalika. Viungo hivi kwa pamoja hata kwa kuwa sehemu mbalimbali katika mwili wa binadamu kwa pamoja huwekwa katika mfumo wa utoaji taka.

Pia sehemu za chini za mfumo wa mmeng'enyo wa chakula kama utumbo mpana zinahesabiwa hapa zikiondoa sehemu ya chakula zisizoweza kutumiwa tena mwilini hadi kutoka kwenye mkundu.

Mapafu na moyo

Utangulizi

[hariri | hariri chanzo]

Wanadamu hula chakula na kunywa maji kwa sababu miili yao hupaswa kulishwa ili isidhoofike wala kuwa na afya mbaya. Lakini katika chakula na maji zimo sehemu nyingine zisizotufaa, na hizi sehemu lazima zitengwe na kutolewa nje ya miili. Kama sehemu hizo hazitolewi tutapatwa na magonjwa na hatimaye tutakufa. Viungo vyenye kazi ya kusafisha mwili ni mapafu, mafigo na ngozi.

Kila kiumbe hai kinahitaji hewa ya oksijeni ili kiweze kuishi. Kila kiumbe kina namna ya kujipatia hewa hii muhimu kwa uhai. Kwa mfano samaki huipata kutoka majini kwa kutumia matamvua, mimea hutumia majani wakati wa usiku. Hali kadhalika wanyama wa jamii ya mamalia hujipatia hewa kwa kutumia mapafu. Binadamu ana mapafu mawili yaliyo ndani ya kifua. Kwa maelezo zaidi kuhusu mapafu angalia mapafu.

Binadamu hutumia hewa ya oksijeni katika kujitengenezea nishati kutoka katika chakula kwa ajili ya matumizi mbalimbali mwilini. Miongoni mwa matokeo ya pambano la chakula na oksijeni pamoja na vimeng’enyo mbalimbali ndani ya seli ya binadamu, pamoja na vitu vingine ni hewa ya carbondioxide. Hewa hii husafirishwa katika damu mpaka ndani ya mapafu ambao huitoa nje kama uchafu ndani ya mwili. Kiwango cha hewa ya carbondioxide kinachotolewa nje kila mtu anapopumua kinaweza kufikia asilimia nne au zaidi za hewa yote inayotolewa nje. Zaidi ya hayo mapafu hutoa maji mengi kwa namna ya mvuke.

Ini ni miongoni mwa ogani muhimu katika mwili wa binadamu. Pia ini ni kimojawapo kati ya viungo vinavyohusika katika kutoa uchafu. Ini hutumika pia katika uhifadhi wa chakula katika mwili wa binadamu. Chakula kinapofonjwa kuingia mwilini katika utumbo mwembamba huelekea kwanza katika ini.

Ini husafisha sumu katika mwili. Kunapokuwa na ongezeko la chakula cha protini, ni jukumu la ini kurekebisha. Uchafu unaotolewa na ini huingizwa katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na hutolewa pamoja na kinyesi.

Ini husafisha pombe, madawa ya kulevya kama heroin, cocaine na mengineyo. Kwa sababu ya jukumu hili la ini, huenda mtu akawa na shida za ini haswa anapotumia vitu vya namna hiyo, hivi kwamba ini linashindwa kudhibiti yale madawa. Shida ya liver cirrhosis ni moja ya magonjwa ya ini.

Wengu (pia "bandama "; kwa Kiingereza spleen) ni kiungo cha mwili chenye nafasi katika mzunguko wa damu. Iko ndani ya fumbatio ya mwili karibu na tumbo. Wengu ya mtu mzima huwa na ukubwa wa takriban sentimita 11 × 7 × 4 na uzito wa gramu 150-200.

Kazi yake ni kuongeza idadi ya seli nyeupe za damu halafu kuondoa seli nyekundu za damu zilizozeeka.

Katika watoto ina pia jukumu la kutengeneza seli nyekundu za damu. Watu wazima kwa kawaida wanaweza kuishi bila wengu.

Mfumo wa mkojo

[hariri | hariri chanzo]
Figo

Katika mwili wa binadamu mafigo yamewekwa nyuma ya tumbo; moja kila upande wa pingili za juu za kiuno. Sehemu ya juu ya mafigo imehifadhiwa kwa jozi mbili za mbavu zinazoelea.

Kila figo kwa umbo lake hufanana na haragwe, lakini kwa ukubwa ni tofauti sana. Figo la kulia kwa kawaida ni fupi na nene zaidi, nalo, kwa sababu ya ini, hukaa chini zaidi kuliko figo la kushoto.

Mafigo yametengenezwa yawe mfano wa chombo cha kuchujia maji. Kazi yake ni kuchuja maji na kutoa uchafu na vitu vyote visivyohitajika mwilini vilivyochukuliwa na damu katika mizunguko yake. Maji hayo pamoja na vitu hafifu vilivyomo ndiyo mkojo.

Mafigo yameshehenezwa na vifereji vilivyonyongwanyongwa, navyo vyote huunganika pamoja kufanya bomba lile litokalo katika kila figo na kufika katika kibofu cha mkojo. Kutoka huko mkojo hutolewa nje kwa mshipa wa kupitia mkojo na uume/uke.

Kibofu cha mkojo

[hariri | hariri chanzo]

Kibofu ni mfuko wa mkojo uliopo mvunguni mwa matumbo. Kwa hiyo mkojo hauwezi kutoka moja kwa moja mara tu unapotengenezwa na mafigo. Kibofu kinapojaa mkojo, mtu huhisi haja ndogo. Kiasi cha mkojo unaotolewa kila siku hubadilika siku hadi siku. Hii hutegemea na hali mbalimbali. Mtu mwenye afya njema hutoa lita moja na nusu hadi lita mbili na nusu za mkojo katika muda wa masaa 24.

Kiasi cha mkojo, huongezeka kama mtu amekunywa sana vinywaji, kwa mfano, pombe, divai, maji ya machungwa au ya mananasi, au kama amepatwa na magonjwa ya figo. Hapa mkojo huwa si wa manjano sana.

Kiasi cha mkojo unaotolewa kila siku hupungua kama mtu hakunywa sana kinywaji cho chote au kama ametokwa na jasho sana. Hali hiyo hutokea pia mtu ashikwapo na homa. Hapo mkojo huwa na rangi ya kimanjano sana, pengine ni wa hudhurungi, na pengine hata kikahawia.

Ngozi ya binadamu

Sehemu ya nje ya mamalia imefunikwa na ngozi. Kutegemeana na mamalia kiwango cha nywele kinachoweza kuota juu ya ngozi kinategemea asili au mahali ambapo mamalia anapatikana. Ngozi ya binadamu inaweza kugawanywa katika sehemu mbili; nazo ni ngozi ya ndani na ngozi ya nje.

Ngozi ya nje

[hariri | hariri chanzo]

Ngozi ya nje ni matabaka mengi ya magamba. Ngozi inaposuguliwa, magamba haya hutoka. Hayo yanaonekana katika ngozi ya kichwa. Matabaka ya chini hayana magamba mengi nayo huwa na rangi maalum ionekanayo katika tofauti za mataifa makuu ya jamii ya wanadamu.

Ngozi ya nje hulinda sehemu za mwili zilizo chini yake na ambazo zina kapilari. Kwa hiyo mtu asiye na ngozi iliyochubuka anaweza kugusa na kutumia vitu vya maji maji vilivyo na sumu asidhurike navyo.

Ngozi ya ndani

[hariri | hariri chanzo]

Ngozi ya ndani au ngozi halisi iko chini au baada ya ngozi ya nje. Ndani ya ngozi ya ndani vimo vinyweleo vya jasho visivyoweza kuhesabika. Karibu na vinyweleo hivyo zipo kapilari. Kila kinyweleo kimefanana na kifereji kilichonyongwanyongwa, na katika kuta zake vimo vifuko vidogo sana kama vile vilivyomo katika mafigo. Vifuko hivyo vinaweza kuondoa uchafu uliomo katika damu na kuupitisha katika vinyweleo mpaka kuutoa nje ya ngozi.

Kwa kawaida jasho huwa halionekani kwa sababu linatoka kwa namna ya mvuke na hutolewa katika hewa. Hapo huitwa jasho lisiloonekana, lakini tukifanya kazi ngumu au kutikiwa na joto sana, basi hapo huwa tunatoa jasho linaloonekana wazi wazi.

Zaidi ya vinyweleo, viko pia vitundu vidogo vingi sana vya malaika, na kila kitundu kina laika yake. Katika vitundu hivyo yamo mafuta, na kazi yake ni kulainisha ngozi isiwe ngumu wala isipasuke kwa baridi.

Kazi ya ngozi

[hariri | hariri chanzo]

Kimsingi ngozi ina kazi mbalimbali. Kwa ufupisho baadhi yake ni kama ilivyofupishwa hapa chiniː

  • Kutupatia mlango wa maarifa yaani kugusa.
  • Kusafisha mwili kwa kutoa nje ya mwili vitu vyote vichafu na visivyohitajika.
  • Kusawazisha joto la mwili.
  • Kulinda kapilari na sehemu zingine zilizomo ndani ya mwili.

Hitimisho

[hariri | hariri chanzo]

Utoaji uchafu katika mwili ni moja kati ya sifa za msingi za kiumbe hai. Inapasa mwili wa kiumbe hai uwe katika uwiano sawa ili uweze kufanya kazi kwa afya bora na kuongeza muda wa kuishi.

Sumu na uchafu ndani ya mwili husababisha kutofanya kazi vizuri na hivyo sehemu mbalimbali za mwili kufa mapema. Afya bora hasa katika ulaji wa mlo kamili inasaidia kwa kiwango kikubwa katika uboreshaji wa viungo hivi muhimu katika kusafisha mwili mzima wa binadamu kwa ndani.

Dhamana ya kusafisha mwili kwa nje kama vile kuuosha kwa maji na kuondoa uchafu unaoachwa nje ya mwili (mfano jasho) na viungo vya ndani, imeachwa kwa kiumbe chote kwa ujumla. Hivyo imetupasa kutunza miili yetu kwa kuiosha kila wakati inapochafuka.

Angalia pia

[hariri | hariri chanzo]
  • Roberts, M. (2000). Advanced Biology, Nelson, London.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Viungo vinavyosafisha mwili kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.