Ufalme wa Mungu
Ufalme wa Mungu (kwa Kiebrania: מלכות malkut, kwa Kigiriki: βασιλεία τοῦ theoũ, basileia tou theou) ni istilahi ya Biblia inayomaanisha kazi ya YHWH (Mungu wa Wanaisraeli) katika Dunia na pia upeo ambamo mapenzi yake yanatimizwa.
Neno hili linafungamana na cheo cha "mfalme" kinachotumiwa kwa YHWH katika Tanakh (Biblia la Kiebrania). Linaonyesha imani kwamba Mungu anatawala juu ya vyote tangu uumbaji na pia kwamba mapenzi ya Mungu yatatekelezwa kote katika siku ya mwisho dhidi ya upinzani wote. Kwa hiyo manabii katika Biblia na maandiko ya kiufunuo huhusisha neno hilo na mawazo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Torati kote duniani, ukombozi wa Wanaisraeli wote kutoka utawala wa kigeni na ukombozi wa mataifa yote kutoka kwa udhalimu, kuja kwa Mungu kwenye hukumu ya mwisho, na mabadiliko ya uumbaji ambayo yatashinda uovu wote pamoja na mateso, maumivu na kifo.
Kulingana na Agano Jipya, Yesu wa Nazareti alitangaza ufalme huu wa Mungu kuwa umekaribia ( Marko 1,15 ). Wanafunzi wake waliona ufalme kwanza katika matendo, kama vile uponyaji wa magonjwa, na mafundisho ya Yesu mwenyewe.
Wakristo wa kwanza waliona kwamba ufalme wa Mungu ulifika katika kazi, kifo na ufufuko wa Yesu. Waliamini kwamba matabiri ya manabii ya Biblia (mfano Isaya 25,8) yalithibitishwa na kuanza kutimizwa katika historia ya Yesu. Maandiko kama Ufunuo 21: yanaonyesha imani hiyo.
Madhehebu ya Ukristo leo yanatofautiana sana katika kuelewa na kueleza mada hiyo.
Tanakh
[hariri | hariri chanzo]Neno "ufalme wa Mungu" linatokana na cheo "mfalme" (Kiebr. מלך melekh ) kikitumiwa kwa ajili ya YHWH. Cheo hicho kilitumika katika historia ya Israeli tangu enzi za wafalme (tangu takriban 1000 KK), hasa katika ibada za Hekalu la Yerusalemu.
Tanakh (Biblia ya Kiebrania, au Agano la Kale) inamtaja "mfalme" YHWH mara kadhaa, kama vile Isaya 6,5, Zaburi 95:1, Zaburi 99:1 na penginepo.
Istilahi "Ufalme wa Mungu" [1] inapatikana mara mbili katika Tanakh (Biblia ya Kiebrania), katika Mambo ya Nyakati I 28:5 [2] na Mambo ya Nyakati II 13:8. Pamoja na hayo, kuna pia maneno “ufalme wake” na “ufalme wako” ilhali hutumiwa kurejelea Mungu.[3] Mifano ni: "Ufalme ni wako, Ee Bwana" jinsi inavyotumika katika Mambo ya Nyakati I 29:10–12 na “Ufalme wake ni ufalme wa milele” katika Danieli 4:3.
Pia kuna mistari kama Kutoka 19:6 inayoonyesha jinsi Israeli, kama watu waliochaguliwa na Mungu, wanavyochukuliwa kuwa ufalme wake.
"Neno la Kiebrania malkuth [...] hurejelea kwanza utawala, na pili tu kwa eneo ambalo utawala unatekelezwa. [...] Wakati malkuth inapotumiwa kuhusu Mungu, karibu kila mara inarejelea mamlaka yake au utawala wake kama Mfalme wa mbinguni."[4]
Agano Jipya
[hariri | hariri chanzo]Katika Agano Jipya, neno la Kigiriki βασιλεία τοῦ Θεοῦ (basileia tou theou, ufalme wa Mungu) linaonekana katika sehemu 122, mara 99 katika Injili Ndugu [5] na mara moja katika Injili ya Yohane ( Yoh 3:3).
Ufalme wa Mungu (au Ufalme wa mbinguni unavyoitwa hasa katika Injili ya Mathayo: βασιλεία τῶν ουρανῶν basileia ton ouranon ) ni mojawapo kati ya mada kuu za ujumbe wa Yesu Kristo katika Injili.[6]
Kufuatana na taarifa za Agano Jipya, Yesu alianza kuonekana hadharani akitangaza ujumbe ambao muhtasari wake ni: "Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili." [7]
Katika mahubiri ya Yesu Ufalme wa Mungu ulionyeshwa kama hali iliyopo tayari: "Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao." [8] Injili zinaonyesha pia imani kwamba ufalme huo ulionekana katika matendo ya Yesu akiponya wagonjwa ("Ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajia."[9]). Kufuatana na Luka 17:21 Ufalme wa Mungu "umo ndani yenu", lakini hakuna ishara zinazoweza kuonyeshwa "huko au kule".[10]
Wengine wameona mvutano katia matamshi ya Yesu kati ya matarajio ya utawala wa Mungu utakaokuja wakati ujao na ishara ya ufalme uliofika tayari. Njia nyingine kuelewa ufalme wa Mungu ni kuuona kama mchakato ulioanza tayari lakini haukukamilika bado. Uelewa huo unaonekana katika Waraka wa kwanza wa Yohane ukisema "Sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa."[11].
Neno "ufalme" (kwa Kigiriki βασιλεία, Basileia) linapatikana mara 162 katika Agano Jipya, kawaida kwa maana ya Basileia tou Theou (βασιλεία τοῦ θεοῦ), Ufalme wa Mungu, au Basileia tōn Ouranōn, (Βασιλεία τῶν Ουρανῶν), Ufalme wa Mbinguni.[12][13]
Hata katika hilo Agano Jipya limeendeleza Agano la Kale, ambapo Mungu anatangazwa kuwa mfalme wa ulimwengu[3][14][15] akiwa na mwakilishi, Daudi na watawala wa ukoo wake, kwa namna ya pekee Masiya, Mwana wa Daudi aliyetarajiwa.
Biblia inatangaza kwamba hatimaye Mungu atawahukumu watu wote kadiri walivyokubali au kukataa mamlaka yake[16]. Juu ya msingi wa madondoo mbalimbali wa Agano Jipya, Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli inathibitisha kwamba hukumu hiyo itafanywa kwa njia ya Yesu. Pia kwa sababu hiyo mwenyewe alipenda kujiita "Mwana wa Mtu" kadiri ya njozi ya Danieli.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Kiebrania מַלְכ֥וּת יְהוָ֖ה malkut YHWH, tafsiri katika matoleo la Kiswahili ni "Ufalme wa BWANA", https://www.bibelwissenschaft.de/online-bibeln/biblia-hebraica-stuttgartensia-bhs/lesen-im-bibeltext/bibelstelle/1. Chronik 28,5/bibel/text/lesen/ch/d30819657841a23db0f38d4a8f7fd7b1/
- ↑ Hapo kwa maana kuwa Israeli ni Ufalme wa Mungu, (Amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa BWANA, juu ya Israeli.). Mambo ya Nyakati I 28:5 SRUVDC https://bible.com/bible/1817/1ch.28.5.SRUVDC
- ↑ 3.0 3.1 France, R. T. (2005). "Kingdom of God". Katika Vanhoozer, Kevin J.; Bartholomew, Craig G.; Treier, Daniel J.; Wright, Nicholas Thomas (whr.). Dictionary for Theological Interpretation of the Bible. Grand Rapids: Baker Book House. ku. 420–422. ISBN 978-0-8010-2694-2. Hitilafu ya kutaja: Invalid
<ref>
tag; name "Wright" defined multiple times with different content - ↑ George Eldon Ladd, The Presence of the Future: The Eschatology of Biblical Realism, Eerdmans (Grand Rapids: 1974), 46–47.
- ↑ Papa Benedikto XVI: Jesus von Nazareth. Von der Taufe im Jordan bis zur Verklärung, Herder, 2007, S. 77, ISBN 3-451-29861-9
- ↑ The Gospel of Matthew by R.T. France (21 Aug 2007) ISBN 080282501X pages 101-103
- ↑ Marko 1:15 https://bible.com/bible/1817/mrk.1.15.SRUVDC
- ↑ Mathayo 5:3 https://bible.com/bible/1817/mat.5.3.SRUVDC
- ↑ Luka 11:20 https://bible.com/bible/1817/luk.11.20.SRUVDC
- ↑ Luka 17:21 https://bible.com/bible/1817/luk.17.21.SRUVDC
- ↑ 1 Yohana 3:2 https://bible.com/bible/1817/1jn.3.2.SRUVDC
- ↑ Theology for the Community of God by Stanley J. Grenz (Jan 31, 2000) ISBN 0802847552 page 473
- ↑ Kingdom of God is translated to Latin as Regnum Dei and Kingdom of Heaven as Regnum caelorum. See A Primer of Ecclesiastical Latin by John F. Collins (Aug 1985) ISBN 0813206677 page 176
- ↑ Dictionary of Biblical Imagery by Leland Ryken, James C. Wilhoit and Tremper Longman III (Nov 11, 1998) ISBN 0830814515 pages 478-479
- ↑ Psalms: Interpretation by James Mays 2011 ISBN 0664234399 pages 438-439
- ↑ "The Hebrew word malkuth [...] refers first to a reign, dominion, or rule and only secondarily to the realm over which a reign is exercised. [...] When malkuth is used of God, it almost always refers to his authority or to his rule as the heavenly King." See George Eldon Ladd, The Presence of the Future: The Eschatology of Biblical Realism, Eerdmans (Grand Rapids: 1974), 46–47.