Suema Akumboke
Suema Akumboke | |
Amezaliwa | Ziwa nyasa, Tanzania |
---|---|
Amekufa | 16 juni 1878 Tanzania |
Nchi | Tanzania |
Kazi yake | alikuwa sista |
Suema Akumboke (alifariki 16 Juni 1878) alikuwa sista wa kwanza mzawa wa eneo la Tanzania ya leo.
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Suema alizaliwa sehemu za ziwa Nyasa. Huko alikamatwa na Waarabu, lakini mama yake hakutaka kuachana naye. Hivyo wote wawili waliingizwa katika msafara wa kupelekwa Unguja na kuuzwa sokoni. Kutokana na urefu na ugumu wa safari mama yake alidhoofika hata Waarabu wakaamua kumuacha porini afe tu. Usiku Suema alitoroka amtafute, lakini asubuhi yake Waarabu waliwafikia. Waliposhindwa kuwatenganisha, mmojawao alimpiga sana yule mama afe peke yake.
Baada ya muda mrefu msafara ulifika Kilwa. Toka huko walikwenda kwa dau mpaka Unguja, lakini Suema alifika hoi, hivyo hakuna aliyetaka kumnunua. Basi, bwana wake aliagiza afungwe katika mkeka na kutupwa shimoni kwenye makaburi kama kwa kuzikwa angali hai. Kumbe usiku huohuo kijana mmoja alipita karibu akasikia kilio cha Suema akamtoa shimoni akampeleka mishenini.
Masista wakampokea na kumtunza. Baadaye alisoma kwa bidii elimu ya shule na ya dini hata akatamani ubatizo, lakini hakuweza kuupata kwa sababu alishindwa kumsamehe Mwarabu aliyemtenda vile mama yake. Kila alipojaribu kusali Baba Yetu aliishia maneno "Utupe leo mkate wetu wa kila siku", asiweze kuendelea "Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea". Masista walimhurumia na kuendelea kumuombea neema ya kusamehe.
Jioni fulani walileta mgonjwa hospitalini, amejeruhiwa vibaya katika ugomvi. Masista walimuita Suema asaidie kutibu majeraha kwa kuleta kitambaa, sahani na vyombo vingine. Alipoingia chumbani na kumuona mgonjwa alishtuka na kuanza kutetemeka hivi kwamba vyote vikachopoka mikononi mwake. Chuki kubwa ilimsonga moyoni kwa kutambua ni Mwarabu aliyemuua mama yake. Hata hivyo sista alipomuomba aokote kila kitu na kumsaidia, Suema polepole akasogea akaanza kumshughulikia yule Mwarabu, hivyo chuki ikaanza kuyeyuka. Kisha kutibu majeraha alikimbilia kanisani. Sista alimfuata akamuona amepiga magoti akikariri kwa machozi ya furaha, "Ee Mungu, Baba mwema, namsamehe, namsamehe!" Basi, juma ileile alibatizwa na kuitwa Magdalena.
Miaka miwili baadaye aliingia shirika la "Mabinti wa Maria" wa Reunion na tarehe 15 Mei 1877 aliweka nadhiri za kitawa akaitwa Sista Maria Antonia. Mwaka uliofuata alifariki dunia.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Kanisa katika Tanzania, V2, Kitabu cha Mwalimu, Ndanda Mission Press, 1975, uk. 28-29
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |