Nyota ya Wolf-Rayet
Nyota ya Wolf-Rayet ni jina la kutaja nyota ambazo ni kubwa na za joto sana. Zimeshapita sehemu kubwa ya maendeleo yake na kupotewa na tabaka za nje za hidrojeni ilhali zinayeyunganisha heliamu au elementi nzito zaidi katika viini vyake ambavyo ni sehemu za pekee zilizobaki.
Zinapoteza masi yake haraka kutokana na mng’aro (en:luminosity) mkali unaotoka kwenye nyota kwa umbo la upepo wa nyota. Ilhali Jua letu linapungua masi za jua 10−14 kila mwaka, nyota za Wolf-Rayet zinapungua M☉ 10−5 kila mwaka kwa njia ya mng’aro, maana nguvu ya mnururisho ndani ya nyota inasukuma gesi ya matabaka ya nje ya nyota itoke kuelekea anga ya nje.[1]
Masi zilizopimwa ziko kati ya M☉ 10 hadi 265. Jotoridi kwenye uso ni kati ya nyuzi za Kelvin 30,000 na 200,000 na hivyo zinazidi karibu nyota zote nyingine.[2]
Mng'aro wake inafikia mara kumi elfu hadi mara milioni mng'aro wa Jua, ingawa si kwa lazima pamoja na mwangaza mkubwa, kwa sababu sehemu kubwa ya mnururisho inaweza kutoka kwenye masafa nje ya nuru inayoonekana, kwa mfano kwenye upeo wa urujuanimno au eksirei.
Mara nyingi nyota za Wolf-Rayet si rahisi kuziangalia kwa sababu kiasi kikubwa cha masi inayotoka kwa njia ya upepo wa nyota inafunika nyota yenyewe.
Nyota hizi zilipokea jina kutoka kwa wanaastronomia wawili Wafaransa Charles Wolf na Georges Rayet waliogundua mwaka 1867 nyota tatu kwenye kundinyota ya Dajaja (Cygnus) zilizoonyesha spektra za pekee.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Ask an astrophysicist: Wolf-Rayet Stars, tovuti ya NASA, iliangaliwa Desemba 2017
- ↑ Sander A; Hamann W.R. & Todt H. 2012. The galactic WC stars. Astronomy & Astrophysics 540: A144. [1]