Maandishi
Maandishi (pia: mwandiko) ni tendo la kushika sauti za lugha kwa njia ya alama zinazoandikwa.
Mitindo ya miandiko
[hariri | hariri chanzo]Sehemu kubwa ya maandishi duniani inatumia alfabeti mbalimbali. Kati yake alfabeti ya Kilatini imesambaa zaidi, ikifuatwa na alfabeti ya Kiarabu na alfabeti ya Kikirili.
Asia ya Mashariki imeendelea kutumia maandishi yake ya alama zinazodokeza neno lote badala ya herufi tu. Mtindo wa kutumia alama kwa neno lote ulitumiwa pia katika utamaduni wa Misri ya Kale na Meksiko ya Kale.
Miandiko ya Uhindi, inayotokana na mwandiko wa Brahmi, hutumia miandiko mbalimbali inayoonyesha silabi. Hata lugha za Ethiopia hufuata mtindo wa kufanana nayo.
Historia ya maandishi
[hariri | hariri chanzo]Hakuna hakika maandishi yalianza lini na wapi. Wataalamu wengi huona ya kwamba Sumer katika Mesopotamia ilikuwa na maandishi ya kwanza duniani.
Wengine huona ya kwamba sanaa ya kuandika ilianzishwa na watu mbalimbali kwa nyakati tofauti katika pande mbalimbali za dunia. Si rahisi kuwa na hakika kwa sababu maandishi yenyewe hudumu kwa muda tu kutegemeana na mata na vifaa vilivyotumiwa.
Maandishi penye mawe magumu tena penye hali ya hewa yabisi hukaa miaka elfu kadhaa. Kwa njia hiyo tuna ushuhuda wa maandishi ya mapema hasa kutoka nchi kama Mesopotamia, Misri, Bara Hindi na China. Lakini hatuwezi kukana uwezekano wa maandishi yaliyotumia mata kama magome ya miti yanayooza haraka hasa katika mazingira yenye mvua nyingi.
Watu waliandika juu ya miamba, vigae vya mwandiko wa kikabari, bao za nta, kitambaa, ubaoni au mabati ya metali mbalimbali. Mainka wa Peru walitumia mwandiko wa mafundo kwenye kamba.
Kati ya mata zote za kutunza maandishi ni hasa karatasi inayotumiwa zaidi leo. Ilibuniwa China ilipojulikana mnamo mwaka 100 BK na kusambaa polepole barani Asia halafu Ulaya.
Siki hizi maandishi ya elektroniki yamesambaa pamoja na matumizi ya tarakilishi na mtandao.