Moshweshwe I
Moshweshwe I alikuwa chifu na mfalme (Kisotho: motlotlehi) wa Basotho katika karne ya 19 tangu 1820 hadi kifo chake mwaka 1870.
Moshweshwe aliunganisha vikundi mbalimbali katika eneo la Lesotho (zamani: Basutoland) akaanzisha taifa la Basotho.
Watu wengi wlikuwa walikimbia Mfecane (vita za Wazulu) wakapata mkimbilio katika milima ya Lesotho ya leo. Tangu 1820 Moshweshwe alifaulu kuwaunganisha na kukubaliwa kama mfalme wao. Alisifiwa kwa hekima yake ya kupatanisha maadui zake baada ya kuwashinda na kuwaunganisha na ufalme wake.
Moshweshwe I. alikuwa na boma lake kwenye Thaba Bosiu (mlima wa usiku) karibu na mahali pa mji Maseru wa leo.
Mfalme alielewa mabadiliko kutokana na silaha za kisasa zilizitumiwa na Makaburu na Waingereza. Aliamua kujipatia ushauri wa Wazungu ambao hawakuwa na mipango ya kisiasa Afrika Kusini akakaribisha Wamisionari Wafaransa Waprotestanti kwake.
Kwa msaada wa washauri wake Wafaransa mfalme alifaulu kutetea uhuru wa eneo lake. Vita mbalimbali zilifuata dhidi ya Waingereza na Makaburu. 1867 Moshweshwe alielewa ya kwamba nchi yake itaharibika na Makaburu waliokuwa waliunda Dola Huru la Mto Orange na kumshambulia vikali. Akaomba ulinzi wa malkia Viktoria I wa Uingereza na nchi yake ikawekwa chini ya ulinzi wa serikali ya Kiingereza iliyozuia mashambulio ya Makaburu.
Moshweshwe aliaga dunia 1870. Hata kama Waingereza walijaribu kuondoa hali ya pekee ya Basutoland na kuiunganisha na koloni ya katika Afrika Kusini upinzani wa wenyeji na kumbukumbu ya ahadi ya malkia vilisaidia kutunza hali ya pekee ya Basutoland iliyokuwa mwishowe nchi huru tangu 1966.
Moshweshwe anakumbukwa na kuheshimiwa kama baba wa taifa.