Nenda kwa yaliyomo

Mnyoo-mjeledi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mnyoo-mjeledi
Jike la mnyoo-mjeledi (Trichuris trichiura)
Jike la mnyoo-mjeledi (Trichuris trichiura)
Dume la mnyoo-mjeledi
Dume la mnyoo-mjeledi
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
(bila tabaka): Bilateria
(bila tabaka): Protostomia
Faila ya juu: Ecdysozoa
Faila: Nematoda
Ngeli: Enoplea
Oda: Trichocephalida
Familia: Trichuridae
Jenasi: Trichuris
Roederer, 1761
Spishi: T. trichiura
(Linnaeus, 1771)

Mnyoo-mjeledi (Trichuris trichiura) ni spishi ya mnyoo kidusia wa familia Trichuridae katika faila Nematoda anayeishi katika sikamu ya watu. Anaweza kusababisha kuhara damu na anemia, katika watoto hasa.

Mofolojia

[hariri | hariri chanzo]

Minyoo-mjeledi wana sehemu nyembamba ya mbele yenye umio na sehemu fupi na nene zaidi ya nyuma. Minyoo hao pinki-nyeupe wamo kama uzi kupitia kiwambo-ute. Wanajiambata na kidusiwa kwa sehemu yao nyembamba ya mbele na hujilisha kwa vinyaa vya tishu badala ya damu. Majike ni wakubwa kuliko madume: urefu wa takriban mm 35-50 kulinganishwa na mm 30-45. Majike wana sehemu ya nyuma nyofu na butu kulinganishwa na wenzao wa kiume wenye sehemu ya nyuma iliyoviringishwa. Dume ana kiunzi kama sindano kinachotokeza kupitia ala ya mviringo yenye miiba na ambayo hutumiwa katika kupandana. Mayai yao bainifu yana umbo la kipipa na rangi ya hudhurungi, na yana kivimbe kwenye ncha zote mbili.

Mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Mnyoo-mjeledi wa kike hutaga mayai 2,000-10,000 yenye seli moja kwa siku. Mayai huenda kutoka kwa kinyesi cha binadamu mpaka kwenye udongo ambapo, baada ya wiki mbili hadi tatu, hupata kiinitete na kuingia katika hatua ya kuambukiza. Mayai haoo humezwa na kutoa lava katika utumbo mwembamba wa binadamu yakitumia flora ya vidubini wa matumbo kama kichocheo cha kutoa lava. Lava hupenya vijidole vya ukuta wa utumbo mwembamba na kuendelea na ukuaji wao, ambao unajumuisha mabambuaji manne. Minyoo wachanga huhamia kwenye sikamu na kupenya kwenye kiwambo-ute, na hapo hukamilisha ukuaji kwa minyoo wapevu ambao huhamia zaidi juu ya utumbo mpana. Mzunguko wa maisha kutoka wakati wa kumeza mayai hadi ukuzaji wa minyoo waliokomaa huchukua takriban miezi mitatu. Wakati huu kunaweza kuwa na ishara ndogo za ambukizo katika sampuli za kinyesi kwa sababu ya ukosefu wa uzalishaji wa mayai na umwagaji wao. Minyoo-mjeledi wa kike huanza kutaga mayai baada ya miezi mitatu ya upevu. Minyoo huishi takriban mwaka mmoja kwa kawaida, wakati ambao majike wanaweza kutaga mayai hadi 20,000 kwa siku.