Nenda kwa yaliyomo

Mwaka

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Miaka)
Mwaka 2024 katika kalenda nyingine
Kalenda ya Gregori 2024
MMXXIV
Kalenda ya Kiyahudi 5784 – 5785
Ab urbe condita (Roma ya Kale) 2777
Kalenda ya Ethiopia 2016 – 2017
Kalenda ya Kiarmenia 1473
ԹՎ ՌՆՀԳ
Kalenda ya Kiislamu 1446 – 1447
Kalenda ya Kiajemi 1402 – 1403
Kalenda za Kihindu
- Vikram Samvat 2079 – 2080
- Shaka Samvat 1946 – 1947
- Kali Yuga 5125 – 5126
Kalenda ya Kichina 4720 – 4721
癸卯 – 甲辰
Analemma ikionyesha mabadiliko ya nafasi ya jua katika kipindi cha mwaka

Mwaka ni kipindi cha takriban siku 365 katika Kalenda ya Gregori ambayo imekuwa kalenda ya kawaida kimataifa ikifuata mwendo wa jua.

Mwaka katika kalenda ya jua

Katika kalenda za jua mwaka unalingana na muda wa mzunguko mmoja wa dunia kwenye mzingo wake kuzunguka jua letu.

Muda kamili wa mzunguko huu ni siku 365.2425.

Kwa sababu hiyo kalenda ya Gregori inaongeza mwaka mrefu wa siku 366 katika utaratibu ufuatao:

  • kila mwaka wa nne utakuwa na siku 366 badala ya 365 kwa kuongeza tarehe 29 Februari. Mifano: 1892, 1996, 2004, 2008, 2012
  • kila mwaka ambao namba yake inagawiwa kwa 100 utakuwa na siku 365 (siyo 366 hata kama namba za miaka hii zinagawiwa kwa 4 pia!). Mifano: 1700, 1800, 1900, 2100
  • kila mwaka ambao namba yake inagawiwa kwa 400 utakuwa tena na siku 366 (siyo 365 hata kama namba za miaka hii zinagawiwa kwa 100 pia!). Mifano: 1600, 2000, 2400, 2800

Miaka katika kalenda mbalimbali

Katika kalenda mbalimbali kuna mahesabu tofauti ya muda wa mwaka.

  • Mwaka wa Kiislamu ni mwaka wa mwezi una siku 354.
  • Mwaka wa Kiyahudi unafuata pia kalenda ya mwezi lakini kwa namna ya pekee ya kuupatanisha na mwendo wa jua; muda wake ni siku 354 lakini kila baada ya miaka miwili au mitatu kuna mwaka mrefu kwa kuongeza mwezi mmoja. Kwa jumla mwezi huingizwa mara 7 katika kipindi cha miaka 19.
  • Kalenda za kihistoria ya Wamaya katika Amerika ya Kati ilikuwa na aina ya mwaka mwenye kipindi cha siku 260 iliyounganishwa na mwaka wa jua wa siku 365 katika utaratibu wa miaka 52.
  • Kalenda ya mwaka wa Kanisa ni kalenda inayoratibu sikuu za kikristo na utaratibu wa liturgia kama vile masomo ya Biblia kwa ajili ibada mbalimbali. Hii ni lazima kwa sababu namna ya kuratibu mwaka si miezi bali wiki na jumapili. Kalenda hii hutofautiana kiasi kati ya makanisa yenye mapokeo ya kiorthodoksi upande mmoja na kanisa katoliki upande mwingine. Waorthodoksi huhesabu kwenye msingi wa kalenda ya Juliasi na Wakatoliki huhesabu kwenye msingi wa kalenda ya Gregori. Makanisa ya kiprotestant kama vile Anglikana na Walutheri hufúata mapokeo ya kikatoliki. Tofauti si muda wa mwaka lakini mwanzo wake. Mwaka wa Kanisa huanza kewenye jumapili ya kwanza ya majilio au Adventi.

Ni kawaida kuwa pia na migawanyiko ya wakati wa mwaka mmoja ambayo si sehemu ya kalenda ya kawaida, kwa mfano:

  • Mwaka wa shule, ambao unaweza kuanza baada ya likizo ndefu za mwaka au kwenye mwezi wa Januari baada ya likizo. Likizo ndefu za mwaka mara nyingi hutokea wakati wa majira ya joto, hivyo mwaka wa shule katika nchi za kaskazini unaanza kwenye Agosti au Septemba. Nchini Tanzania kuna mwaka wa shule za msingi hadi O-level unaoanza Januari, halafu mwaka wa A-level na Chuo unaoanza mwezi wa Julai[1].
  • Mwaka wa fedha ni kipindi cha mwaka mmoja ambao ni wakati wa kutoa taarifa za fedha, makadirio ya kodi au ya bajeti ya serikali. Unategemea mfumo uliowekwa kwa sheria au mapokeo ya kila nchi.

Marejeo

  1. Tanzania's school system - an overview, tovuti ya africaid, iliangaliwa Septemba 2022