Maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya
Maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya (kwa Kiingereza/Kigiriki: Holocaust, kwa Kiebrania Shoah השואה) yalikuwa mauaji ya Wayahudi milioni 5-6 wa Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya miaka 1940 na 1945. Mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na serikali ya Ujerumani chini ya Adolf Hitler kwa msaada wa serikali za nchi zilizofungamana na Ujerumani au zilizokuwa chini ya jeshi la Ujerumani.
Mauaji hayo yalitekelezwa kwa njia ya
- kuwapiga watu risasi,
- kuwafunga katika makambi bila chakula wala dawa hadi wafe kwa njaa na
- kuwaua kwa gesi ya sumu katika makambi maalumu.
Utangulizi wa maangamizi makuu
Utangulizi wa maangamizi makuu ulitokea nchini Ujerumani tangu chama cha NSDAP cha Hitler kushika serikali mwaka 1933. Sheria zilitangazwa zilizotenga Wayahudi katika jamii. Kabla ya vita shabaha ya hatua hizo ilikuwa kuwatesa na kuwalazimisha waondoke katika Ujerumani.
- 1933: Wayahudi walikataliwa kuwa watumishi wa umma, Wayahudi na wote wenye asili ya Kiyahudi walifukuzwa katika utumishi. Rais Hindenburg alidai utaratibu maalum kwa Wayahudi waliokuwa wanajeshi Wajerumani wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia eti wabaki jinsi walivyokuwa. Baada ya kifo chake utaratibu huu ulupuuzwa pia.
- 1935: Sheria mbalimbali ziliondoa haki za kiraia za Wajerumani Wayahudi:
- Walizuiliwa kufanya kazi mbalimbali
- Waliondolewa haki ya kupiga kura katika uchaguzi
- Harusi kati ya Wahayudi na wasio Wayahudi zilipigwa marufuku kama kila tendo la kutwaana kati yao nje ya harusi
- Sheria ilweka utaratibu ni nani atakayetazamiwa kuwa Myahudi kamili, nusu Myahudi ao robo Myahudi kulingana na idadi ya wazazi au mababu Wayahudi.
- 1938:
- Wayahudi wa kisheria walipaswa kuongeza majina ya "Israel" (wanaume) au "Sara" (wanawake) katika vitambulisho vyao
- Wajerumani wasio Wayahudi walikataliwa kufanya kazi katika maduka au makampuni ya Wayahudi
- Wayahudi walipaswa kuandikisha mali yao yote serikalini - hii ilikuwa utangulizi wa uporaji wao wa baadaye
- Wayahudi walikataliwa misaada ya serikali kwa ugonjwa au matatizo mengine
- Madaktari na wenye duka la dawa walikataliwa kuwahudumia wasio Wayahudi
- Wanafunzi Wayahudi walifukuzwa katika shule za serikali
- 9 na 10 Novemba masinagogi yaliangamizwa kote Ujerumani, nyumba nyingi za Wayahudi zilivunjwa na wanaume wengi kufungwa jela; jumuiya ya Kiyahudi ya Ujerumani ililazimishwa kuchangia bilioni moja ya Mark kwa serikali ya Ujerumani
- Wayahudi walikataliwa kuendesha maduka au makampuni ya kila aina au kusimamia kazini wasio Wayahudi kama wakubwa wao.
Mwaka 1933 katika Ujerumani waliishi Wayahudi 510,000. Hadi mwaka 1939 takriban 315,000 waliondoka nyumbani. Kati ya 200,000 waliobaki takriban 15,000 waliweza kukimbia mwaka huo. Wengine 10,000 walifaulu kubaki katika Ujerumani mara nyingi mafichoni. Wote wengine walikufa katika maangamizi makuu kuanzia mwaka 1941.
Kutoka ubaguzi na mateso hadi maangamizi
Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilianza 1 Septemba 1939 kwa uvamizi wa Poland. Poland ilikuwa na mamilioni ya raia wa Kiyahudi waliojikuta ghafla chini ya utawala wa Kijerumani.
Mipango ya kwanza ya viongozi wa NSDAP ilikuwa kupeleka Wayahudi wote wa Ujerumani Poland na kukusanya Wayahudi wote wa Poland katika mkoa maalumu ndani ya nchi. Mkurugenzi wa mipango hii alikuwa kiongozi mkuu wa SS Heinrich Himmler aliyepewa cheo cha "kamishna kwa uzawa wa Kijerumani". Ilionekana haraka ya kwamba idadi kubwa ya watu ilishinda uwezo wa Himmler hasa kuwapa nyumba na chakula.
Vita dhidi ya Urusi na azimio la maangamizi makuu
Baada ya kuanza vita dhidi ya Urusi imeshaonekana ya kwamba Wanazi walishindwa kushughulika idadi kubwa ya Wayahudi katika maeneo ya Ulaya ya Mashariki yaliyotekwa na Ujerumani. Kufuatana na itikadi yao walitaka kuwatenga Wayahudi na watu wengine lakini
waka 1941 Wajerumani walishambulia Urusi walipokuta tena mamilioni ya raia wa Kiyahudi. Himmler aliyeona ya kwamba siasa ya kuwakusanya mahali pamoja ilishindikana hasa kuwapatia nyumba na kuwalisha. Pia ilionekana kwa viongozi wa juu ya kwamba vita dhidi ya Urusi haikuenda jinsi ilivyopangwa na kuingia kwa Marekani vitani kuliongeza matatizo. Katika hali hii wakati wa mwisho wa 1941 / mwanzo wa 1942 walichukua hatua ya kuamua kile walichoita "usuluhisho wa mwisho wa suala la Kiyahudi" yaani mauaji wa Wayahudi wote wa Ulaya.
Mauaji ya kwanza
Himmler alianza majaribio na vikosi maalumu vya kuwaua Wayahudi. Vikosi hivi walikuwa mapolisi kutoka Ujerumani, vikundi vya SS pamoja na wasaidizi wenyeji kutoka nchi zilizovamiwa. Vikosi hivi walifuata jeshi la kawaida wakakusanya Wayahudi katika miji na kuwaua kwa kuwapiga risasi.
Makambi ya mauti
Himmler aliona ugumu wa kuwaua watu wengi sana kwa njia hiyo. Hapa alikata shauri ya kuanzisha makambi ya mauti kwa lengo la kuwaua kikiwandani.
Wayahudi walikusanywa kote katika Ulaya ya Mashariki na kupelekwa kwa treni kwa makambi ya KZ. Mwisho wa safari ulikuwa makambi ya mauti kama vile:
- Chelmno – Kulmhof
- Auschwitz
- Belzec
- Sobibor
- Treblinka
- Majdanek
- Maly Trostinez
Zote zilijengwa nje ya eneo la Ujerumani penyewe, sita katika Poland na moja katika Belarusi. Viongozi wa Nazi waliona Wajerumani wenyewe wasijue kwa undani habari za mauaji kwa sababu waliogopa upingamizi. Lakini watu wa Poland walitazamiwa kama watumwa kwa hiyo waliona nchi hii inafaa. Mahali palichaguliwa karibu na reli. Kwa njia hiyo iliwezekana kuwasafirisha Wayahudi wa Poland na Urusi lakini pia kutoka Ufaransa, Italia, Uholanzi na Ulaya ya Kusini.
Baada ya safari ndefu katika mabehewa ya mifugo wafungwa walitoka wakaangaliwa na madaktari mara moja mbele ya treni. Wenye afya waliwekwa kando na kupelekwa katika sehemu ya kambi ambako walipaswa kufanya kazi kama watumwa katika viwanda vilivyojengwa huko hasa. Wengine kama wagonjwa, wazee na watoto pamoja na wakinamama walitengwa na kuambiwa kuingia katika chumba kikubwa cha bafu chenye 210 m² walipotakiwa kujisafisha baada ya safari ndefu. Milango ikafungwa na gesi ya sumu badala ya maji ikaingizwa katika chumba kupitia vifaa vya manyunyu. Waliokufa walikuwa watu 500-700 kila safari. Maiti zikatolewa; midomo ikachunguliwa kama mtu alikuwa na dhahabu kwenye meno iliyotolewa halafu maiti zikachomwa katika meko makubwa.
Katika makambi sita za aina hii jumla ya watu milioni 2-3 waliuawa. Pamoja na wale waliouawa nje ya makambi ni mnamo watu milioni sita waliouawa kikusidi. Walio wengi sana walikuwa Wayahudi lakini pia vikundi vingine visivyolingana na itikadi ya kimbari kama vile Wasinti, walemavu, shoga na wafungwa wakomunisti.
Mwisho wa makambi
Mauaji katika makambi yalisimamishwa kwa sababu jeshi la Ujerumani lilianza kushindwa vitani likarudi nyuma. Jeshi la Umoja wa Kisoveyti likakaribia makambi ya mauti wakati wa majira ya baridi ya 1944/45. Wakuu wa SS walijaribu kuficha matendo yao ilivyowezekana. Kuanzia mwisho wa 1943 makambi ndani ya Urusi na mashariki ya Poland yalibomolewa, mabaki ya maiti yalitolewa kwenye mashimo ya makaburi halafu kuchomwa na mifupa yalisagwa ilikuficha dalili zote za mauaji. Katika sehemu ambako makambi yaliendelea hadi 1945 wafungwa wenye afya walipelekwa kwa safari ndefu kwa miguu bila chakula na bila makoti katika baridi kali. Kila moja aliyeshindwa kutembea aliuawa. Wagonjwa walibaki katika makambi walipopatikana wakati Warusi walipofika. Walipofika Auschwitz tar. 27 Januari 1945 meko ya kuchoma maiti bado yalikuwa moto. Watu waliendelea kufa hata baada ya uhuru wao kufika kwa sababu wengi walikuwa wadhaifu mno.
Wayahudi wachache walibaki au kurudi tena Poland au Ujerumani; wengi waliondoka ama kwenda Marekani au nchi mpya ya Israel.
Maadhimisho
Matukio ya mauaji hayo huadhimishwa kila mwaka katika nchi nyingi kwenye tareke 27 Januari kama Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya (International Holocaust Remembrance Day) kufuatana na azimio la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye mwaka 2005.
Tanbihi
Viungo vya nje
- The trials of an American Prosecutor Archived 16 Aprili 2008 at the Wayback Machine.
- Women guards in Bergen-Belsen
- Teaching alternatives Archived 13 Julai 2007 at the Wayback Machine.
- http://www1.yadvashem.org/Odot/prog/index_before_change_table.asp?gate=0-2 Archived 5 Juni 2011 at the Wayback Machine.
- The destruction of European Jews (English Wikipedia)
- Shoah (film)