Abu Bakr
Abu Bakr (kwa Kar.: أبو بكر Abū Bakr al-Ṣiddīq; Makka, 573 kwa jina la ʿAbd Allah; Madina, 23 Agosti 634) alikuwa khalifa wa kwanza katika Uislamu baada ya kifo cha Mtume Muhammad. Alikuwa baba wa Aisha, mke mdogo wa Muhammad.
Abu Bakr alikuwa kati ya wafuasi wa Mtume Muhammad walioshikamana naye tangu mwanzo na kuongozana naye wakati wa hijra.
Baada ya kifo cha mtume huyo alichaguliwa kuwa kiongozi mpya kwa msaada wa Umar ibn al-Khattab na Wakuraish. Abu Bakr akatumia cheo cha "mfuasi wa mtume wa Allah" (khalifatu-rasuli-llah) au khalifa.
Kati ya kazi zake za kwanza ilikuwa vita za riddah dhidi ya makabila ya Waarabu walioona ya kwamba baada ya kifo cha Muhammad hawakuwa na wajibu kwa kiongozi mpya. Wengine walikataa malipo ya zakat, wengine walirudia dini zao za awali.
Baada ya kushinda vita hizi Abu Bakr alituma jeshi lake dhidi ya Bizanti na Uajemi. Hapo kaskazini Waarabu walikutana na milki mbili kubwa zilizochoka baada ya vita ya mnamo mwaka wa 30 kati yao. Zaidi ya hapo Wajemi walikuwa katika kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe. Jemadari Khalid bin Walid alishambulia Hira katika Mesopotamia na upande wa Bizanti jeshi la Waarabu likaingia katika Palestina.
Kwa upande wa dini Abu Bakr alimpa Umar bin Khattab kazi ya kukusanya mapokeo ya Korani. Kabla ya kuaga dunia alimtaja Umar kama mwandamizi wake. Alifariki mjini Madinamnamo mwaka 634 akazikwa kando ya Muhammad katika Masjid al Nabawi.